UJASILIAMALI


UMASKINI NA CHANZO CHAKE

CHANZO KIKUU CHA UMASKINI WA TANZANIA

 Miaka nenda miaka rudi, taifa la Tanzania limeeendelea kuhesabika miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani. Sio tu kuhesabika uko kwa taifa hili kuko katika takwimu za wataalamu wa uchumi, bali pia kiwango cha maisha ya watanzania wengi ni cha chini sana.

Watanzania tumeeendelea kuishi maisha ya dhiki sana, mulo kwa wengi kuupata imekuwa taabu, nyumba wanamoishi watu ni hohehahe, elimu ya wengi wetu ni duni, kusafiri toka sehemu moja hadi nyingine shida tupu (vijijini na mijini), huduma za afya licha ya kutopatikana kwa urahisi, zilizopo wanaomudu gharama zake ni wachache na hata hivyo hazilidhishi, vipato vya wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara viko hoi, ili mradi tu ni dhiki juu ya nyingine.

 Wakati walio wengi taabu zetu kwa kutaja chache ndio hizo, wapo wenzetu wachache nchini ambao maisha yao ni ya neema, tena neema tele. Watanzania tumeendelea kujiuliza, kulikoni bila majibu. Baadhi yetu tu, mfano wasomi na wengine,

 wamejaribu kutafuta majibu na ufumbuzi wa umaskini huu lakini hadi sasa bila suluhisho. Kwa kutumia nadharia kwa mfano, wapo wanaosema chanzo na kiendelezo cha umaskini wetu, ni tabia ya watanzania wengi kutojiwekea akiba, yaani baada ya kuzalisha kidogo, kidogo hicho chote kinawekwa katika matumizi, hivyo hakuna akiba na kwahiyo hakuna uwekezaji katika mradi wowote mpya wa uzalishaji au kupanua uliopo, na matokeo yake uzalishaji unaendelea kuwa kidogo kama sio kupungua, ilimradi unakuwa ni mduara tatizi usiokoma wa ufukara.

 Kwa kusimamia kwenye nadharia hii, wapo wanaotuhubiria watanzania kwamba tujenge tabia ya kuweka akiba jamani. Ni mahubiri mazuri sana, lakini swali la kujiuliza hapo ni je, kweli kuna mtanzania asiyetaka kuweka akiba?

Kwa maoni yangu, mtanzania wa hivyo hajazaliwa, bali sisi tunaoishi roho zetu zi radhi kuweka akiba lakini hali halisi inakataa. 

Wengi watakubaliana nami kwamba, mfanyakazi wa Tanzania ya leo ambaye mara nyingi mshahara wake wa mwezi huisha siku kumi au kumi na tano baada ya kuupokea, kumwambia aweke akiba ni kumkejeli mchana kweupe!

Mfanyakazi wa kitanzania, maisha yake yamejaa madeni kwenye maduka ya rejareja. Laiti kama mikopo anayochukua kwenye maduka hayo ingekuwa ya bidhaa za ziada, sio, ni madeni yatokanayo na mahitaji ya sukari, chumvi, sabuni, sembe na bidhaa nyingine za namna hiyo. 

Kilio cha wafanyakazi hawa kimeendelea kuwa ni kile kile mwaka hadi mwaka, wakidhani tatizo ni kwamba mshahara hautoshi. Watawala wetu katika kujibu malalamiko ya mishahara kutotosha, wamekuwa wakifurahisha mikutano wanayoihutubia kwa kuimba ngonjera ile ile, ‘Mwaka huu wa bajeti tutaongeza mishahara’ mara kadhaa wanaongeza kweli.
Nyongeza hizo licha ya kuwa kiduchu zimeendelea kutotatua tatizo, bado mshahara hautoshi na hauelekei kama utatosha siku za karibuni. Kumbe shida ni nini hasa? 

Wengine wakasema ni kwa sababu kuna mfumko wa bei, kiasi kwamba nyongeza inapotoka tayari bidhaa madukani zimepanda mara dufu na huduma za jamii zimeenda juu vile vile.

Kwa upande mwingine yapo madai kwamba umasikini wetu pengine unatokana na uvivu wa watanzania (hili linasemwa sana na wabaguzi ambo mara kadhaa wamedai eti sisi waafrika ni wavivu). 

Bado naendelea kujiuliza kama hilo lina chembe zozote za ukweli, ili kama hilo ndio tatizo la Tanzania, tusione aibu kulikiri na hivyo kuamua kuondokana nalo.

Lakini haiingi akilini kirahisi kwamba watanzania tunaofanya kazi kutwa kucha, usiku na mchana, siku za kawaida, mwisho wa wiki na hata kwenye sikukuu hadi wengine tunaitwa walalahoi, bado tunaweza kuambiwa uvivu ndio sababu ya umaskini wetu.

MAENEO YA VIJIJINI
Maeneo ya vijijini, mkulima masikini anamka kabla ya jogoo kuwika ili awahi shambani, inamlazimu wakati mwingine kushinda njaa ili asirejee nyumbani na kuharibu kazi aliyokusudia kuimaliza siku hiyo.

Msimu wote wa kilimo, mvua yake, jua kali lake na taabu nyinginezo za maporini. Maskini mkulima huyu kapinda mgongo na jembe lake la mkono ili mkono uende kinywani.

 Tena anapaswa alime kwa bidii hata mazao ya biashara ili apate fedha, maskini mazao yake miaka nenda miaka rudi hayapati bei inayolingana japo angalau na nguvu kazi yake aliyotumia. Bado mtu huyu aambiwe wewe ni maskini kwa sababu ya uvivu? Kadhalika kwa wafanyakazi, nitolee mfano walimu; mwalimu anayedamka asubuhi na mapema sambamba na wanafunzi wake, akafanya kazi zake siku nzima ya kazi, na kwa kuwa hazikuisha akabebana nazo kwenda nyumbani, ili usiku awashe kibatali na kuzimalizia (hana tofauti na Kayumba), baada ya hapo aandae anafundisha nini kesho, wakati wanafunzi wake wako likizo yeye ndio kwanza anasahihisha mitihani yao na kuandaa mpangokazi wa muhula unaofuata.

Huyu naye aambiwe sababu ya umaskini wake ni uvivu, kweli? Aidha upo mtizamo kwamba, sababu ya kuendelea kwetu kuwa masikini ni kwa kuwa watanzania tunamiliki mali lakini hazina urasmi, yamkini wa kutuwezesha kupata mikopo toka taasisi za fedha na kadhalika.

 Ndio maana ukaja huu makakati wa kurasmisha mali hizo kama harakati mojawapo ya kupambana na ufukara nchini. Sambamba na hilo, ipo dhana ya kwamba mikopo kwa watu binafsi na vikundi vya jamii itatuokoa ufukarani. 

Kwa sababu hiyo sasa tuna mamilioni ya Kikwete na mikopo mingine! Maswali bado ni mengi hapo. Ni nini kinaweza kutokea kwa mfano, iwapo watanzania watachukua hiyo mikopo midogo midogo na hatimaye kugeuka taifa la wachuuzi, tena wa bidhaa zitokazo nje, umaskini utaondoka? Uchumi utakua?

 La hasha, maana bado mimi naamini kutokuwepo kwa mikopo hiyo bado sio sababu ya umaskini wa wananchi.

 Hata hivyo kuwepo kwake, si hatua ya kubeza. Katika harakati za kutusaidia, tumehimizwa sana kuwekeza popote fursa inapojitokeza, mfano kununua hisa katika makampuni au mashirika.

 Hili limefanyika sana. Watanzania tunakumbuka pia Rais mstaaafu wa awamu ya tatu alivyotuhutubia siku moja, kwamba tofauti yetu na matajiri wa nje, hususan wanaokuja nchini kuwekeza ni kwamba waliona mapema umuhimu wa hisa, na kwa kuzinunua ndiko walikopata mitaji yao wanayoihamishia sasa nchini ketu ili wachume zaidi. Hivyo akatushauri tuone haja ya kununua hisa kama kweli tunataka kuondokana na umasikini.

Lakini bado tunarudi kulekule, yule mwenye mshahara usiomfikisha mwisho wa mwezi, au ambaye mazao yake hayajanunuliwa na ambaye mwenye duka anamdai, kapata wapi cha kununulia hisa. Tumeedelea kujiuliza zaidi na zaidi juu ya chanzo na suluhu ya umaskini wetu. Wapo wanaodhani kwamba sisi ni maskini kwa majaliwa ya maumbile.
Sisi ni maskini kwa sababu taifa letu halikuumbwa tajiri kama yalivyo mataifa mengine. Hili ndio kwanza halina hata lepe la ukweli.

 TANZANIA NI NCHI TAJIRI

 Tanzania kwa asili ni nchi tajiri sana! Tena ingefaa watanzania tutambue na kujivunia ukweli huo kwamba nchi yetu imependelewa muno kuliko nchi nyingi sana duniani. Utajiri wetu wa maliasili hauna mfano.
Tuna eneo kubwa sana la ardhi tena yenye rutuba, ifaayo kwa kilimo na shughuli nyinginezo za kiuchumi. Yapo mataifa ambayo watu wake si maskini kwa kiwango chetu, lakini ardhi yao waliyojaliwa ni jangwa. Hapo asomaye na afahamu ni kwa nini Namibia fedha yao ina nguvu sana ukilinganisha na ya kwetu.
Tanzania tumejaliwa madini na vito vya thamani vingi sana, na vingine havipatikani popote ulimwenguni ila Tanzania tu. Kuitaja Tanzanite kumezoeleka, watanzania tufahamu pia kwamba licha ya dhahabu, almasi, bati, taja madini yoote yang’aayo na yasiyon’gaa utayakuta nchini. Ni sisi pekee vile vile tuliojaliwa madini ambayo walioyagundua waliamua kuyaita Nyerereite kwa sababu ya upekee wake duniani. Kana kwamba hilo halitoshi,
 wakati wenzetu wanalia kwa kukosa maji, sisi kila mahali ni mito na maziwa makubwa yanayopendeza hata kwa mpangilio na mtandao wake nchi nzima. Ziwa kubwa kuliko yote Afrika liko Tanzania, Ziwa lenye kina kirefu kuliko yote Afrika nalo liko Tanzania! Ndio maana mojawapo ya nyimbo zetu za kizalendo tunasema, tazama ramani utaona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka!
Aidha wakati mataifa mengine, yamefungiwa ndani kwa ndani kiusafiri, sisi tuna pwani ya bahari ya Hindi yenye kilometa nyingi za urefu na bandari kadhaa zinazotuhudumia wenyewe na mataifa jirani yanazitumia tena kwa kutulipa fedha nyingi tu za ushuru. Mshangao uaongezeka tunapoambiwa mataifa hayo hayo yanayotutegemea katika sekta hiyo, yanatuzidi kiuchumi. Tuseme nini kuhusu baraka ya misitu na wanyama na vivutio vingine vya utalii. Utajiri wetu katika eneo hilo umeyatia wivu mataifa mengi ambayo hayana, lakini mataifa hayo hayo watu wake si fukara kama sisi. Kulikoni? Baba wa taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutueleza, tunahitaji watu ili kuiendeleza nchi yetu.

Ingawa hitaji la watu si tu kwamba wawe wengi bali pia wawe na maarifa na maadili, sisi Tanzania tumejaliwa hata katika hilo. Jamani, kwa sasa twapata milioni arobaini (40), lakini nchi zenye wakazi kidogo tu zinatuzidi mbali kiuchumi.
Unakuta nchi kwa ujumla ina idadi ya watu sawa na wakazi wa Dar es salaam peke yake au pungufu, lakini maendeleo yao hatuwafikii hata robo. Labda nidokezee tu kwamba, idadi ya wakazi nchini Finland kwa mfano, ni milioni tano na ushee kidogo.
Namibia nilikotolea mfano wa kwanza, kuna watu wasiozidi milioni mbili. Tuseme nini basi, wingi wetu ndio unaotuponza? La hasha, ingawa kwa mtazamo mwingine idadi kubwa ya watu wasio na mwelekeo ni tatizo. Litupasalo sisi ni kuutumia vizuri wingi huo, kuuondoa katika umaskini ili kila mmoja wetu azidi kuwa wa manufaa kwa taifa. Mataifa mengine, yametumia wingi wao kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo.
Kinachotakiwa ni kuwa na watu walio bora, kwa maana ya wenye elimu, afya na uwezo wa kutenda. Umasikini umekuwa chanzo cha wananchi wetu kuwa na elimu duni na afya zisizolidhisha. Bahati mbaya baadhi ya waliobahatika kupata elimu nzuri wamekimbilia nchi za nje kwa sababu ya maslahi duni yanayotolewa hapa nchini.
Tuna bahati mbaya kwamba watanzania wenzetu hao wametoa mchango mkubwa sana katika kutokomeza umasikini wa nchi za wenzetu, ilihali nyumbani (kama ulivyo msemo wa mitaani) kumedoda. Hoja yangu hapo ni kwamba, wingi wetu si chanzo cha umasikini bali ni baraka ambayo laiti tungeitumia vizuri, Tanzania ingehesabika katika ulimwengu wa kwanza. Mtazamo mwingine juu ya umasikini wetu, ni ule unaoona kwamba sababu zake si za ndani bali zinatoka nje.
 Mtazamo huu unauhusianisha umasikini na ukoloni tulioupitia katika historia ya nchi yetu. Kwamba kwa kutawaliwa na wakoloni wa kijerumani na baadaye waingereza, tulinyonywa na tunaendelea kunyonywa kupitia ukoloni mambo leo, utandawazi na uwekezaji wa kigeni. Hapa pana ukweli wa kiasi chake, japo hapatoshi kuwa sababu hasa inayoeleza chanzo cha ufukara nchini, na wala suluhu yake haitakuja kwa kupambana tu na mkoloni wa zamani na wa sasa. Mataifa kadhaa ulimenguni yalipitia kutawaliwa na wakoloni kama sisi, lakini leo hii wao (sio wote) si masikini kama sisi. Hapa nirudie mfano wa Finland iliyotawaliwa na Urusi na Sweden, au nchi za Asia zilizokuwa makoloni ya mwingereza.
 Walijikomboa kutoka ukoloni, wakakaa chini kizalendo wakajenga nchi zao, umaskini ukatokomea. “kwani wao waliweza wana nini, na sisi tunashindwa ni kwanini?” Hata hivyo hatuwezi kupuuza hujuma za nchi zinazojifanya viranja wa ulimwengu, hususan nchi za magharibi dhidi ya nchi changa.
Hawa hawa ndio wanaendelea kutuharibia kwa kutupangia nini tufanye na nini tuache. Wanaendelea pia kushirikana na wazandiki wasioitakia nchi yetu mema bali nafsi zao, japo ni watanzania wenzetu. Ndio hao aliowasema Baba wa taifa, kwamba ni miti (mipini) iliyomo kwenye mashoka ya chuma inayowakata akina miti. (shoka bila mpini halikati mti, ati)
Hivyo, tunapoendelea kuulaumu/ kuusingizia ukoloni na utandawazi tusisahau kuwatazama Yuda Iskariote wetu. Wenzetu hao ni sababu mojawapo ya kudumu kwa umaskini wetu, na nadhani kwa kuwadhibiti tutaudhibiti umasikini vilevile.
MANENO YA VIONGOZI WETU
 Wakati fulani nimepata kusikia baadhi ya viongozi wetu wakitaja kuwa, sisi ni masikini kwa sababu kadhaa, mojawapo ni vita tulivyopigana dhidi ya Idd Amin wa Uganda mnamo mwaka 1978/79 (miaka therathini imepita sasa) Mnh, binafsi sipuuzi athari za vita hiyo, lakini kuitaja kama sababu ya umasikini kukithiri nchini, ni kukosa kisingizio, kujisemea tu au kuogopa kujinyooshea kidole. Jamani, vita hiyo imepiganwa muda mrefu umepita sasa, tena ilidumu kwa miezi sita tu.
Watasemaje majirani zetu wa Rwanda na Burundi ambao kwa sasa nchi zao (hasa Rwanda) zinatengemaa kiuchumi, na ajabu Faranga yao ina nguvu kuliko Shilingi ya Tanzania. Namibia wamepata uhuru mwaka 1990 jamani, vita vya ukombozi huko vilidumu kwa muda, ilihali sisi tulipata uhuru bila damu. Uhuru wetu wa bila kumwaga damu na utulivu wetu (wengine wanasema amani,amani umasikinini?) wa muda mrefu, zilikuwa ni sababu tosha za sisi kuwa mbali sana kimaendeleo kuliko wenzetu wengi.
Mungu atupe nini ndugu zangu. Wapo vile vile wanaosema, watanzania hasa vijana, ni maskini kwa sababu ya ukosefu wa ajira. Tatizo la ajira miongoni mwa vijana kweli lipo, lakini kimantiki halikupaswa kuwepo. Katika enzi hizi za sayansi na teknolojia, ambamo matumizi ya maarifa yameongezeka, nchi yetu inatajwa kuwa mojawapo ya nchi zisizo na raslimaliwatu yenye kumudu hayo.
Hivyo tatizo si kwamba ajira hazipo, ila vijana hawana elimu. Nchi yetu vile vile inazo sekta ambazo wengi wanaoziendesha nguvu zao sasa zinaelekea machweo. Matharani sekta ya kilimo, kwa kuwa inaonekana kutokuwa na tija, vijana wanaikimbia na kuwaachia wazee vijijini. Laiti kama sekta hiyo ingebadilishwa sura yake ya sasa, wimbo wa hakuna ajira ungewekwa makumbusho. Laiti kama elimu ingetolewa kwa vijana wote hawa, tena elimu iliyo sahihi,
Tanzania isingekuwa tena mahali ambapo mwekezaji kutoka nje anawakosa wenyeji wenye taaluma na ujuzi unaoendana na biashara/shughuli yake, inamlazimu kuja na wataalamu wake. Niliyoyajadili hapo juu, si mapya sana. Haja ya kuyataja inajitokeza kwa ajili ya kujenga mazingira ya hoja yangu kuu, na vile vile kulitazama suala la umasikini, chanzo chake na suluhu yake kwa mapana zaidi. Juhudi nyingi watanzania tumefanya,
 lakini umasikini umeendelea kusimama wima kama mlima Sayuni unaosemekana hautatikisika kamwe. Au kama Mbuyu katika mbuga za Dodoma.
Tumefika mahali tumegundua kisababishi kikuu cha uamsikini wetu, na hicho ndio ninataka tukiangalie leo kwa makini ili hatimaye tuchukue hatua sahihi na mwisho umaskini nchini ugeuke historia ( tena isiyojirudia)



                                            MWISHO

No comments:

Post a Comment