JIFUNZE KISWAHILI
Changamkia fursa ya Lugha ya Kiswahili
UJASILIAMALI
UMASKINI NA CHANZO CHAKE
CHANZO
KIKUU CHA UMASKINI WA TANZANIA
Miaka nenda miaka rudi, taifa la Tanzania
limeeendelea kuhesabika miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani. Sio tu
kuhesabika uko kwa taifa hili kuko katika takwimu za wataalamu wa uchumi, bali
pia kiwango cha maisha ya watanzania wengi ni cha chini sana.
Watanzania tumeeendelea kuishi maisha ya dhiki sana, mulo
kwa wengi kuupata imekuwa taabu, nyumba wanamoishi watu ni hohehahe, elimu ya
wengi wetu ni duni, kusafiri toka sehemu moja hadi nyingine shida tupu
(vijijini na mijini), huduma za afya licha ya kutopatikana kwa urahisi,
zilizopo wanaomudu gharama zake ni wachache na hata hivyo hazilidhishi, vipato
vya wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara viko hoi, ili mradi tu ni dhiki
juu ya nyingine.
Wakati walio wengi
taabu zetu kwa kutaja chache ndio hizo, wapo wenzetu wachache nchini ambao
maisha yao ni ya neema, tena neema tele. Watanzania tumeendelea kujiuliza,
kulikoni bila majibu. Baadhi yetu tu, mfano wasomi na wengine,
wamejaribu kutafuta majibu na ufumbuzi wa umaskini
huu lakini hadi sasa bila suluhisho. Kwa kutumia nadharia kwa mfano, wapo
wanaosema chanzo na kiendelezo cha umaskini wetu, ni tabia ya watanzania wengi
kutojiwekea akiba, yaani baada ya kuzalisha kidogo, kidogo hicho chote
kinawekwa katika matumizi, hivyo hakuna akiba na kwahiyo hakuna uwekezaji
katika mradi wowote mpya wa uzalishaji au kupanua uliopo, na matokeo yake
uzalishaji unaendelea kuwa kidogo kama sio kupungua, ilimradi unakuwa ni mduara
tatizi usiokoma wa ufukara.
Kwa kusimamia kwenye
nadharia hii, wapo wanaotuhubiria watanzania kwamba tujenge tabia ya kuweka
akiba jamani. Ni mahubiri mazuri sana, lakini swali la kujiuliza hapo ni je,
kweli kuna mtanzania asiyetaka kuweka akiba?
Kwa maoni yangu, mtanzania wa hivyo hajazaliwa, bali sisi
tunaoishi roho zetu zi radhi kuweka akiba lakini hali halisi inakataa.
Wengi
watakubaliana nami kwamba, mfanyakazi wa Tanzania ya leo ambaye mara nyingi
mshahara wake wa mwezi huisha siku kumi au kumi na tano baada ya kuupokea, kumwambia
aweke akiba ni kumkejeli mchana kweupe!
Mfanyakazi wa kitanzania, maisha yake yamejaa madeni kwenye
maduka ya rejareja. Laiti kama mikopo anayochukua kwenye maduka hayo ingekuwa
ya bidhaa za ziada, sio, ni madeni yatokanayo na mahitaji ya sukari, chumvi,
sabuni, sembe na bidhaa nyingine za namna hiyo.
Kilio cha wafanyakazi hawa
kimeendelea kuwa ni kile kile mwaka hadi mwaka, wakidhani tatizo ni kwamba
mshahara hautoshi. Watawala wetu katika kujibu malalamiko ya mishahara
kutotosha, wamekuwa wakifurahisha mikutano wanayoihutubia kwa kuimba ngonjera
ile ile, ‘Mwaka huu wa bajeti tutaongeza mishahara’ mara kadhaa wanaongeza
kweli.
Nyongeza hizo licha ya kuwa kiduchu zimeendelea kutotatua
tatizo, bado mshahara hautoshi na hauelekei kama utatosha siku za karibuni.
Kumbe shida ni nini hasa?
Wengine wakasema ni kwa sababu kuna mfumko wa bei,
kiasi kwamba nyongeza inapotoka tayari bidhaa madukani zimepanda mara dufu na
huduma za jamii zimeenda juu vile vile.
Kwa upande mwingine yapo madai kwamba umasikini wetu
pengine unatokana na uvivu wa watanzania (hili linasemwa sana na wabaguzi ambo
mara kadhaa wamedai eti sisi waafrika ni wavivu).
Bado naendelea kujiuliza kama
hilo lina chembe zozote za ukweli, ili kama hilo ndio tatizo la Tanzania,
tusione aibu kulikiri na hivyo kuamua kuondokana nalo.
Lakini haiingi akilini kirahisi kwamba watanzania
tunaofanya kazi kutwa kucha, usiku na mchana, siku za kawaida, mwisho wa wiki
na hata kwenye sikukuu hadi wengine tunaitwa walalahoi, bado tunaweza kuambiwa
uvivu ndio sababu ya umaskini wetu.
MAENEO
YA VIJIJINI
Maeneo
ya vijijini, mkulima masikini anamka kabla ya jogoo kuwika ili awahi shambani,
inamlazimu wakati mwingine kushinda njaa ili asirejee nyumbani na kuharibu kazi
aliyokusudia kuimaliza siku hiyo.
Msimu
wote wa kilimo, mvua yake, jua kali lake na taabu nyinginezo za maporini.
Maskini mkulima huyu kapinda mgongo na jembe lake la mkono ili mkono uende
kinywani.
Tena anapaswa alime kwa bidii hata mazao ya
biashara ili apate fedha, maskini mazao yake miaka nenda miaka rudi hayapati
bei inayolingana japo angalau na nguvu kazi yake aliyotumia. Bado mtu huyu
aambiwe wewe ni maskini kwa sababu ya uvivu? Kadhalika kwa wafanyakazi, nitolee
mfano walimu; mwalimu anayedamka asubuhi na mapema sambamba na wanafunzi wake, akafanya
kazi zake siku nzima ya kazi, na kwa kuwa hazikuisha akabebana nazo kwenda
nyumbani, ili usiku awashe kibatali na kuzimalizia (hana tofauti na Kayumba),
baada ya hapo aandae anafundisha nini kesho, wakati wanafunzi wake wako likizo
yeye ndio kwanza anasahihisha mitihani yao na kuandaa mpangokazi wa muhula
unaofuata.
Huyu
naye aambiwe sababu ya umaskini wake ni uvivu, kweli? Aidha upo mtizamo kwamba,
sababu ya kuendelea kwetu kuwa masikini ni kwa kuwa watanzania tunamiliki mali
lakini hazina urasmi, yamkini wa kutuwezesha kupata mikopo toka taasisi za
fedha na kadhalika.
Ndio
maana ukaja huu makakati wa kurasmisha mali hizo kama harakati mojawapo ya
kupambana na ufukara nchini. Sambamba na hilo, ipo dhana ya kwamba mikopo kwa
watu binafsi na vikundi vya jamii itatuokoa ufukarani.
Kwa sababu hiyo sasa
tuna mamilioni ya Kikwete na mikopo mingine! Maswali bado ni mengi hapo. Ni
nini kinaweza kutokea kwa mfano, iwapo watanzania watachukua hiyo mikopo midogo
midogo na hatimaye kugeuka taifa la wachuuzi, tena wa bidhaa zitokazo nje,
umaskini utaondoka? Uchumi utakua?
La hasha, maana bado mimi naamini kutokuwepo
kwa mikopo hiyo bado sio sababu ya umaskini wa wananchi.
Hata
hivyo kuwepo kwake, si hatua ya kubeza. Katika harakati za kutusaidia, tumehimizwa
sana kuwekeza popote fursa inapojitokeza, mfano kununua hisa katika makampuni
au mashirika.
Hili limefanyika sana. Watanzania tunakumbuka
pia Rais mstaaafu wa awamu ya tatu alivyotuhutubia siku moja, kwamba tofauti
yetu na matajiri wa nje, hususan wanaokuja nchini kuwekeza ni kwamba waliona
mapema umuhimu wa hisa, na kwa kuzinunua ndiko walikopata mitaji yao
wanayoihamishia sasa nchini ketu ili wachume zaidi. Hivyo akatushauri tuone
haja ya kununua hisa kama kweli tunataka kuondokana na umasikini.
Lakini
bado tunarudi kulekule, yule mwenye mshahara usiomfikisha mwisho wa mwezi, au
ambaye mazao yake hayajanunuliwa na ambaye mwenye duka anamdai, kapata wapi cha
kununulia hisa. Tumeedelea kujiuliza zaidi na zaidi juu ya chanzo na suluhu ya
umaskini wetu. Wapo wanaodhani kwamba sisi ni maskini kwa majaliwa ya maumbile.
Sisi
ni maskini kwa sababu taifa letu halikuumbwa tajiri kama yalivyo mataifa
mengine. Hili ndio kwanza halina hata lepe la ukweli.
TANZANIA NI NCHI TAJIRI
Tanzania
kwa asili ni nchi tajiri sana! Tena ingefaa watanzania tutambue na kujivunia
ukweli huo kwamba nchi yetu imependelewa muno kuliko nchi nyingi sana duniani.
Utajiri wetu wa maliasili hauna mfano.
Tuna
eneo kubwa sana la ardhi tena yenye rutuba, ifaayo kwa kilimo na shughuli
nyinginezo za kiuchumi. Yapo mataifa ambayo watu wake si maskini kwa kiwango
chetu, lakini ardhi yao waliyojaliwa ni jangwa. Hapo asomaye na afahamu ni kwa
nini Namibia fedha yao ina nguvu sana ukilinganisha na ya kwetu.
Tanzania
tumejaliwa madini na vito vya thamani vingi sana, na vingine havipatikani
popote ulimwenguni ila Tanzania tu. Kuitaja Tanzanite kumezoeleka, watanzania
tufahamu pia kwamba licha ya dhahabu, almasi, bati, taja madini yoote yang’aayo
na yasiyon’gaa utayakuta nchini. Ni sisi pekee vile vile tuliojaliwa madini
ambayo walioyagundua waliamua kuyaita Nyerereite kwa sababu ya upekee wake
duniani. Kana kwamba hilo halitoshi,
wakati
wenzetu wanalia kwa kukosa maji, sisi kila mahali ni mito na maziwa makubwa
yanayopendeza hata kwa mpangilio na mtandao wake nchi nzima. Ziwa kubwa kuliko
yote Afrika liko Tanzania, Ziwa lenye kina kirefu kuliko yote Afrika nalo liko
Tanzania! Ndio maana mojawapo ya nyimbo zetu za kizalendo tunasema, tazama
ramani utaona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka!
Aidha
wakati mataifa mengine, yamefungiwa ndani kwa ndani kiusafiri, sisi tuna pwani
ya bahari ya Hindi yenye kilometa nyingi za urefu na bandari kadhaa
zinazotuhudumia wenyewe na mataifa jirani yanazitumia tena kwa kutulipa fedha
nyingi tu za ushuru. Mshangao uaongezeka tunapoambiwa mataifa hayo hayo
yanayotutegemea katika sekta hiyo, yanatuzidi kiuchumi. Tuseme nini kuhusu
baraka ya misitu na wanyama na vivutio vingine vya utalii. Utajiri wetu katika
eneo hilo umeyatia wivu mataifa mengi ambayo hayana, lakini mataifa hayo hayo
watu wake si fukara kama sisi. Kulikoni? Baba wa taifa Marehemu Mwalimu Julius
Nyerere aliwahi kutueleza, tunahitaji watu ili kuiendeleza nchi yetu.
Ingawa
hitaji la watu si tu kwamba wawe wengi bali pia wawe na maarifa na maadili,
sisi Tanzania tumejaliwa hata katika hilo. Jamani, kwa sasa twapata milioni
arobaini (40), lakini nchi zenye wakazi kidogo tu zinatuzidi mbali kiuchumi.
Unakuta
nchi kwa ujumla ina idadi ya watu sawa na wakazi wa Dar es salaam peke yake au
pungufu, lakini maendeleo yao hatuwafikii hata robo. Labda nidokezee tu kwamba,
idadi ya wakazi nchini Finland kwa mfano, ni milioni tano na ushee kidogo.
Namibia
nilikotolea mfano wa kwanza, kuna watu wasiozidi milioni mbili. Tuseme nini
basi, wingi wetu ndio unaotuponza? La hasha, ingawa kwa mtazamo mwingine idadi
kubwa ya watu wasio na mwelekeo ni tatizo. Litupasalo sisi ni kuutumia vizuri
wingi huo, kuuondoa katika umaskini ili kila mmoja wetu azidi kuwa wa manufaa
kwa taifa. Mataifa mengine, yametumia wingi wao kupiga hatua kubwa sana
kimaendeleo.
Kinachotakiwa
ni kuwa na watu walio bora, kwa maana ya wenye elimu, afya na uwezo wa kutenda.
Umasikini umekuwa chanzo cha wananchi wetu kuwa na elimu duni na afya
zisizolidhisha. Bahati mbaya baadhi ya waliobahatika kupata elimu nzuri
wamekimbilia nchi za nje kwa sababu ya maslahi duni yanayotolewa hapa nchini.
Tuna
bahati mbaya kwamba watanzania wenzetu hao wametoa mchango mkubwa sana katika
kutokomeza umasikini wa nchi za wenzetu, ilihali nyumbani (kama ulivyo msemo wa
mitaani) kumedoda. Hoja yangu hapo ni kwamba, wingi wetu si chanzo cha
umasikini bali ni baraka ambayo laiti tungeitumia vizuri, Tanzania ingehesabika
katika ulimwengu wa kwanza. Mtazamo mwingine juu ya umasikini wetu, ni ule
unaoona kwamba sababu zake si za ndani bali zinatoka nje.
Mtazamo
huu unauhusianisha umasikini na ukoloni tulioupitia katika historia ya nchi
yetu. Kwamba kwa kutawaliwa na wakoloni wa kijerumani na baadaye waingereza,
tulinyonywa na tunaendelea kunyonywa kupitia ukoloni mambo leo, utandawazi na
uwekezaji wa kigeni. Hapa pana ukweli wa kiasi chake, japo hapatoshi kuwa
sababu hasa inayoeleza chanzo cha ufukara nchini, na wala suluhu yake haitakuja
kwa kupambana tu na mkoloni wa zamani na wa sasa. Mataifa kadhaa ulimenguni
yalipitia kutawaliwa na wakoloni kama sisi, lakini leo hii wao (sio wote) si
masikini kama sisi. Hapa nirudie mfano wa Finland iliyotawaliwa na Urusi na
Sweden, au nchi za Asia zilizokuwa makoloni ya mwingereza.
Walijikomboa
kutoka ukoloni, wakakaa chini kizalendo wakajenga nchi zao, umaskini
ukatokomea. “kwani wao waliweza wana nini, na sisi tunashindwa ni kwanini?”
Hata hivyo hatuwezi kupuuza hujuma za nchi zinazojifanya viranja wa ulimwengu,
hususan nchi za magharibi dhidi ya nchi changa.
Hawa
hawa ndio wanaendelea kutuharibia kwa kutupangia nini tufanye na nini tuache.
Wanaendelea pia kushirikana na wazandiki wasioitakia nchi yetu mema bali nafsi
zao, japo ni watanzania wenzetu. Ndio hao aliowasema Baba wa taifa, kwamba ni
miti (mipini) iliyomo kwenye mashoka ya chuma inayowakata akina miti. (shoka
bila mpini halikati mti, ati)
Hivyo,
tunapoendelea kuulaumu/ kuusingizia ukoloni na utandawazi tusisahau kuwatazama
Yuda Iskariote wetu. Wenzetu hao ni sababu mojawapo ya kudumu kwa umaskini
wetu, na nadhani kwa kuwadhibiti tutaudhibiti umasikini vilevile.
MANENO
YA VIONGOZI WETU
Wakati
fulani nimepata kusikia baadhi ya viongozi wetu wakitaja kuwa, sisi ni masikini
kwa sababu kadhaa, mojawapo ni vita tulivyopigana dhidi ya Idd Amin wa Uganda
mnamo mwaka 1978/79 (miaka therathini imepita sasa) Mnh, binafsi sipuuzi athari
za vita hiyo, lakini kuitaja kama sababu ya umasikini kukithiri nchini, ni
kukosa kisingizio, kujisemea tu au kuogopa kujinyooshea kidole. Jamani, vita
hiyo imepiganwa muda mrefu umepita sasa, tena ilidumu kwa miezi sita tu.
Watasemaje
majirani zetu wa Rwanda na Burundi ambao kwa sasa nchi zao (hasa Rwanda)
zinatengemaa kiuchumi, na ajabu Faranga yao ina nguvu kuliko Shilingi ya
Tanzania. Namibia wamepata uhuru mwaka 1990 jamani, vita vya ukombozi huko vilidumu
kwa muda, ilihali sisi tulipata uhuru bila damu. Uhuru wetu wa bila kumwaga
damu na utulivu wetu (wengine wanasema amani,amani umasikinini?) wa muda mrefu,
zilikuwa ni sababu tosha za sisi kuwa mbali sana kimaendeleo kuliko wenzetu
wengi.
Mungu
atupe nini ndugu zangu. Wapo vile vile wanaosema, watanzania hasa vijana, ni
maskini kwa sababu ya ukosefu wa ajira. Tatizo la ajira miongoni mwa vijana
kweli lipo, lakini kimantiki halikupaswa kuwepo. Katika enzi hizi za sayansi na
teknolojia, ambamo matumizi ya maarifa yameongezeka, nchi yetu inatajwa kuwa
mojawapo ya nchi zisizo na raslimaliwatu yenye kumudu hayo.
Hivyo
tatizo si kwamba ajira hazipo, ila vijana hawana elimu. Nchi yetu vile vile
inazo sekta ambazo wengi wanaoziendesha nguvu zao sasa zinaelekea machweo.
Matharani sekta ya kilimo, kwa kuwa inaonekana kutokuwa na tija, vijana
wanaikimbia na kuwaachia wazee vijijini. Laiti kama sekta hiyo ingebadilishwa
sura yake ya sasa, wimbo wa hakuna ajira ungewekwa makumbusho. Laiti kama elimu
ingetolewa kwa vijana wote hawa, tena elimu iliyo sahihi,
Tanzania
isingekuwa tena mahali ambapo mwekezaji kutoka nje anawakosa wenyeji wenye
taaluma na ujuzi unaoendana na biashara/shughuli yake, inamlazimu kuja na
wataalamu wake. Niliyoyajadili hapo juu, si mapya sana. Haja ya kuyataja
inajitokeza kwa ajili ya kujenga mazingira ya hoja yangu kuu, na vile vile
kulitazama suala la umasikini, chanzo chake na suluhu yake kwa mapana zaidi.
Juhudi nyingi watanzania tumefanya,
lakini
umasikini umeendelea kusimama wima kama mlima Sayuni unaosemekana hautatikisika
kamwe. Au kama Mbuyu katika mbuga za Dodoma.
Tumefika
mahali tumegundua kisababishi kikuu cha uamsikini wetu, na hicho ndio ninataka
tukiangalie leo kwa makini ili hatimaye tuchukue hatua sahihi na mwisho
umaskini nchini ugeuke historia ( tena isiyojirudia)
MWISHO
Subscribe to:
Comments (Atom)
-
UMASKINI NA CHANZO CHAKE CHANZO KIKUU CHA UMASKINI WA TANZANIA Miaka nenda miaka rudi, taifa la Tanzania limeeendelea kuhesabika ...